Sunday, 19 April 2015

MGOMO WA MADREVA WANUKIA TENA

Serikali imerejesha mafunzo ya madereva kila baada ya miaka mitatu wakati wa kumalizika kwa muda wa leseni zao, huku ikifafanua kuwa elimu watakayoipata ina umuhimu katika kazi zao, kutokana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea katika sekta hiyo.
 
Naibu Waziri wa Kazi na Ajira, Makongoro Mahanga, alitangaza uamuzi huo wa Serikali jana katika mkutano kati yake na viongozi wa madereva wa mabasi nchini.

Mkutano huo umefanyika kama ilivyoahidiwa na Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka, wakati alipokuwa akijitahidi kumaliza mgomo wa madereva uliofanyika Aprili 10 mwaka huu, wakati walipokuwa wakipinga pamoja na mambo mengine, sharti la kwenda shule ili kupata leseni mpya.

Madereva hao walitaka Serikali ifanyie marekebisho Sheria ya Usalama Barabarani, kwa kuondoa kipengele kinachowataka madereva kwenda Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT)kwa mafunzo ya muda mfupi kila wakati leseni zao zinapoisha, ili kupata sifa ya kupata leseni nyingine.

Sababu ya kupinga kupata mafunzo, ilidaiwa kuwa utaratibu huo uliotangazwa Machi 30, mwaka huu, ulianzishwa bila kushirikisha madereva katika kuuandaa.

Pia walipinga kutakiwa kujilipia gharama za shule hiyo ambazo walidai ni Sh 560,000 kwa magari ya kawaida na Sh 200,000 kwa magari ya abiria.

Sababu nyingine iliyochangia wapinge shule hiyo, walidai ni kukosekana kwa mikataba ya ajira, inayoweza kuwahakikishia kulindwa kwa kazi zao hadi wanapomaliza mafunzo.

Madai mengine yaliyokuwa nje ya shule hiyo, madereva hao walitaka kuondolewa kwa faini ya Sh 300,000 kwa kila kosa la barabarani na kuitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (SUMATRA), kuhakiki uhalisia wa dereva anayeandikishwa na mmiliki wa chombo husika.

Majibu ya Serikali Mahanga aliyekuwa Mwenyekiti wa kikao hicho, alisoma tamko la Serikali lililoeleza kuwa pamoja na kurejesha mafunzo hayo, utekelezaji wake hautafanyika mara moja kwa kuwa Kanuni zake hazijakamilika.
 
“Tangazo hili (la kwenda shule) limetolewa kwa kuzingatia umuhimu wa mafunzo kazini kwa wafanyakazi na madereva kama ilivyo kwa wafanyakazi wengine,” Mahanga. 

Alisisitiza kuwa baada ya miaka mitatu ya leseni, dereva atatakiwa kupata mafunzo mafupi, ambayo ni kati ya siku tatu hadi saba na atakayegharimia mafunzo hayo ni mwajiri, si mfanyakazi na ni katika chuo chochote kinachotambulika.

Akifafanua, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Ndani, Mwamini Malemialiyekuwepo katika mkutano huo, alisema mitaala ya mafunzo hayo bado inaandaliwa, hivyo si rahisi Kanuni hiyo kuanza kutekelezwa mwaka huu hata kama zitakamilika.

Kuhusu mikataba ya ajira ambayo ililalamikiwa mno na madereva wakati wa mgomo, Mahanga alisema Serikali itapitia upya mikataba hiyo ili kuhakikisha mambo yote muhimu yanazingatiwa.
 
Akiongezea hoja katika suala la mikataba, Malemi alisema ni lazima mikataba iwe imekamilika kabla ya kuanza kutumika kwa kanuni ya kwenda shule, ili ioneshe wajibu wa mwajiri katika kumsomesha mfanyakazi.

Kuhusu kauli iliyotolewa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,Suleiman Kova ya kuondoa tochi za kupima mwendo kasi barabarani, Mahanga alisema matumizi ya tochi zinazotumika kupima mwendo kasi na ratiba ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria za Usalama Barabarani

No comments:

Post a Comment